Wednesday, September 6, 2017

UPENDO WA MUNGU KWETU



UPENDO WA MUNGU KWETU

Baba wa mbinguni anatupenda si kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili yetu; bali alimtoa mwana wake kufa kwa sababu anatupenda. Kupitia kwa Kristo Mungu alimimina pendo lake lisilo kifani kwenye ulimwengu uliojawa na dhambi. “yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” 2 Kor 5:19. Kupitia maumivu ya Gethsemani na kifo cha msalaba, Mungu alilipa gharama ya ukombozi wetu.
Yesu alisema, “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena” Yohn 10:17. Hii ni kusema kwamba, “Baba yangu aliwapenda mno kiasi cha kunipenda mimi zaidi pale nilipoutoa uhai wangu kuwakomboa. Nalikufa badala yenu, nilichukua dhabi zenu. Kwa sababu hii, nimekuwa karibu zaidi na Baba yangu kuliko awali, na hata sasa Mungu bado anaokoa wenye dhambi wote waniaminio.”

Kwa kumtoa mwanawe kufa kwa ajili yetu, Baba yetu wa mbinguni alitoa kafara kuu na kulipa gharama ya wokovu wetu. Gharama hii kubwa yapaswa kutusaidia kuelewa kile Mungu anachotegemea sisi kuwa kupitia kwa Kristo.
Mtume Yohana aliona jinsi kimo, kina na mapana ya upendo wa Mungu vilivyo. Alijaribu kuuzungumzia lakini hakuweza kuwa na maneno sahihi ya kuuelezea, na hivyo akasema, “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.” 1 Yohn 3:1. Sisi ni wa thamani kiasi gani!

Kwa kufikiri juu ya upendo wa Mungu tunanyenyekezwa. Wazo hili, kama lilivyooneshwa na kifo cha Yesu, linapaswa kusogeza akili zetu karibu na Mungu. Kwa kadri tunavyojifunza tabia ya Mungu na kudumu kuutazama msalaba, ndivyo tunavyozidi kuona rehema, upole na msamaha wa Mungu. Ndivyo pia tunavyoona Mungu ni wa haki kiasi gani. Pia tunaona upendo wake usio na mwisho na huruma yake inayozidi huruma ya mama kwa mtoto asiye mtiifu.

No comments:

Post a Comment