MAOMBI
MUNGU huzungumza nasi kupitia
katika viumbe vyake vya asili na mafunuo
yake, kupitia katika maongozi yake,
na kwa njia ya Roho wake. Lakini njia hizo
hazitoshi; sisi pia tunahitaji
kumfungulia mioyo yetu. Ili tupate uzima wa kiroho na
nguvu yake, hatuna budi kuongea na
Baba yetu aliye mbinguni. Mawazo yetu yanaweza
kuvutwa kwake; tunaweza
kuzitafakari kazi zake, rehema zake, baraka zake; lakini
hayo, kwa maana yake kamili, si
kuongea naye. Ili tuweze kuongea na Mungu, ni sharti
tuwe na mambo fulani ya kumwambia
hasa kuhusu maisha yetu tunayoishi.
Katika kuomba tunamfunulia Mungu
mioyo yetu na kuongea naye kama
tunavyoongea na rafiki wa kweli. Si
lazima kufanya hivyo ili kumjulisha Mungu hali
yetu ilivyo, bali kuongea naye
kunatuwezesha kumpokea mioyoni mwetu. Maombi
hayamlazimishi Mungu kushuka kwetu,
bali ni sisi ambao tunainuliwa mpaka kufika
kwake.
Yesu alipokuwapo hapa duniani,
aliwafundisha wanafunzi wake kusali.
Aliwaagiza waweke mahitaji yao ya
kila siku mbele za Mungu, na kumtwika mizigo yao
yote. Na ahadi ile aliyowapa kwamba
dua zao zingesikilizwa ni ahadi iliyotolewa kwetu
pia.
Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni,
nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
kwa maana kila aombaye hupokea;
naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa (Mathayo 7:7,8).