Kama
tutasikiliza tu, basi, viumbe vilivyoumbwa na Mungu vitatufundisha mafundisho
ya thamani juu ya utii na kumtegemea yeye. Kuanzia na nyota ambazo zinafuata njia
zao zisizo na alama katika anga za juu na kizazi kwa kizazi zinafuata njia yao
ziliyowekewa, mpaka chini kwenye atomu ndogo kabisa, viumbe vya asili huyatii mapenzi
ya Muumbaji. Tena Mungu hukitunza na kukilisha kila kitu alichokiumba. Yule anayeyashikilia
malimwengu yasiyohesabika katika eneo kubwa sana, wakati uo huo anajali
mahitaji ya shomoro mdogo wa kikahawia aimbaye wimbo wake mdogo pasipo hofu.
Wanadamu
wanapoondoka asubuhi kwenda kazini, na wakati waombapo; wakati wanapokwenda
kulala usiku; na wakati wanapoamka asubuhi; tajiri anapofanya karamu katika
jumba lake, au maskini anapowakusanya watoto wake kukizunguka chakula chao kidogo,
kila mmoja huangaliwa kwa huruma na upendo na Baba yetu aliye mbinguni. Hakuna
chozi limtokalo mtu ambalo Mungu halioni. Hakuna tabasamu yo yote asiyoiona.
Kama
tungesadiki hivyo kabisa, mahangaiko yote yasiyofaa yangeondolewa mioyoni
mwetu. Maisha yetu yasingejazwa na kukata tamaa mno kama yalivyo sasa; kwa
sababu kila kitu, kiwe kikubwa au kidogo, kingeachwa mikononi mwake Mungu, ambaye
hachanganyikiwi kuona ongezeko kubwa la masumbufu yetu, wala halemewi na mizigo
yake. Hapo ndipo tungeweza kuifurahia amani mioyoni mwetu ambayo kwa wengi kwa
muda mrefu imekuwa kitu kigeni.
Mungu
husema nasi katika matendo yake na uongozi wake, tena katika mvuto wa Roho wake
mioyoni mwetu. Katika mambo yanayotokea kwetu, na katika mazingira yetu, katika
mabadiliko yanayotokea kila siku pande zote, twaweza kupata mafundisho ya
thamani, kama mioyo yetu imekuwa wazi kuyatambua mafundisho hayo. Mtunga Zaburi,
akifuatilia matendo na uongozi wa Mungu, asema hivi, “Nchi imejaa fadhili za Bwana.” “Aliye
na hekima na ayaangalie hayo, na wazitafakari fadhili za Bwana.” Zaburi 33:5; 107:43.
_Njia Salama Sura ya 10.
Kama umebarikiwa na ujumbe huu na ungependa kujifunza zaidi, waweza kuweka comment hapo chini au kuwasiliana nasi kupitia ilalasda@gmail.com

No comments:
Post a Comment