JE UNAMJUA MUNGU?
“Mimi ndimi mchungaji mwema;
nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;” Yohana 10:14
atika sura
ya 3 ya kitabu cha 1 Samweli, tunapata habari za kuitwa kwa nabii Samweli tangu
akiwa mtoto. Samweli alikuwa ni mtoto wa ahadi aliyetolewa wakfu kwa Mungu.
Ijapokuwa alitolewa wakfu kwa Mungu na alikuwa akifanya kazi hekaluni, Samweli
hakumjua BWANA, tena hakuitambua sauti ya BWANA.
“Basi
Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado
halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka
akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya
kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto”. 1 Samweli 3: 7-8
Swali kwetu
leo: Je, tunamjua Mungu? Je, tunamtambua? Tunasikiliza sauti gani katika maisha
yetu? Mungu anapozungumza nasi Je, tunaitambua sauti yake?
Ni hatari
sana kuwa kwa BWANA na wakati hatuijui sauti yake kwa maana ni rahisi
kuifananisha na sauti nyingine. Samweli aliifananisha sauti ya BWANA na sauti
ya kuhani Eli.
Kitu kizuri
cha kutia moyo ni kwamba, ijapokuwa hakumtambua BWANA, Samweli alikuwa tayari
kujifunza kuhusu Mungu.
“Bwana
akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli
akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia”. 1 Samweli 3:10
Swali kwetu
leo: Je, ni mara ngapi tunatafuta kumjua BWANA kupitia neno lake?
Pasipo
kusoma neno, kuna hatari ya kupoteza mwelekeo na hivyo kutomtambua BWANA.
Pia katika
kitabu cha Matendo 9 kuna kisa cha Sauli aliyebadilika na kuwa Paulo. Sauli
alijifuza elimu ya dini vizuri na kufikia kiwango cha mafarisayo. Watu
walimwamini na kutegemea makuu toka kwake. Wengine walimtegemea kama kiongozi
mkuu na mfundishaji mzuri wa elimu ya dini katika jamii ya wayahudi.
Kisha Sauli
alipewa kazi ya kuwatafuta, kuwatesa na kuwaua watu wa Mungu walioonekana kuwa
wazushi. Sauli alidhani kuwa anafanya kazi ya BWANA, kumbe alikuwa akimwudhi.
Sauli hakutambua sauti ya BWANA. Ijapokuwa hakumtambua BWANA, alipoisikia sauti
yake ikisema naye, alikubali na kuwa na utayari wa kumpendeza na kumtii.
Huenda kwetu
mimi na wewe, isingetosha kwa kuisikia sauti tu, kuamini kwamba ni sauti ya Mungu.
Yohana 10:14
inasema “Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu
wanijua mimi.”
Swali kwetu
leo: Je, Mungu anatujua kama tulio wa kwake? Je, Mungu anatujua kama alivyomjua
Ayubu, Daudi, Ibrahimu n.k.?
BWANA
ameweka kila njia ya sisi kumfahamu Yeye. Tunao uchaguzi, BWANA halazimishi
tumfahamu ila anataka tumfahamu. Ametupatia neno, alilipa deni kwa ajili yetu,
ametupa Roho wake kutusaidia na anaendelea kutuombea.
Ikiwa
tutatumia muda mwingi kutazama, kusikia na kusimulia kwa uzuri habari za dunia
kuliko kutafuta habari za Yesu, macho yetu ya kiroho yatafumbwa na kamwe
hatutaweza kumtambua BWANA.
Mathayo
11:28-29 inasema “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na
mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi
ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”
Tunaye
mchungaji mwema Yesu Kristo anataka kutuongoza na kubadili maisha yetu. Yesu
anatuita sote kujisalimisha kwake. Kwake tutajifunza na kupata raha nafsini mwetu.
No comments:
Post a Comment